Mwakilishi wa wadi ya Sensi ilioko eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini Kaunti ya Kisii Ochong’a Nyagaka, amewaomba wahisani wema kujitolea kuungana pamoja kutoa usaidizi kwa watoto mayatima kutoka vijiji mbalimbali katika wadi hiyo ili kuwasomesha watoto hao.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Marani, alopokuwa anatembelea miradi yake ya maendeleo katika wadi hiyo, mwakilishi huyo aliomba watu kujitolea na kuungana pamoja kuwasaidia mayatima kwa kuwasomesha ili wapate elimu ambayo itawasaidia watoto hao nyakati za usoni.
“Tukiungana kama jamii, watoto mayatima katika wadi hii hawatakuwa na shida wanapoendelea kupata masomo yao. Naomba wahisani wajitolee tuungane tutoe msaada kwa watoto hawa,” alisema Nyagaka.
Wakati huo huo, mwakilshi huyo alisema elimu ndio itafanya mtu kujulikana nchini na hata kupata kazi na kuomba wototo wote katika wadi hiyo kutia bidii katika masomo.
Mwakilishi huyo pia alitumia fursa hiyo kuomba wazazi kuwasomesha watoto wao ili waweze kujisaidia katika siku za usoni.
“Wazazi wenzangu, mtoto huwa mtu wa kuheshimika katika jamii kwasababu ya masomo na ni jukumu la kila mzazi kumpeleka mtoto wake shuleni ili kupata mafunzo ,” aliongeza Ochong’a.
Mwakilishi huyo alisema masomo ni bure katika shule za msingi na hata watoto hufanya mitihani bila kulipishwa.
“Kazi ya mzazi ni kumnunulia mtoto wako sare za shule na kumlisha vizuri ili asome. Naomba wahisani wema katika wadi hii yangu wajitolee tuwanunulie watoto mayatima sare za shule ili nao wapate fursa ya kusoma kama wengine," alisema Ochong’a.