Share news tips with us here at Hivisasa

Madereva wa magari ya aina mbalimbali mjini Kisii wamewaomba maafisa wa trafiki mjini humo kuboresha uelekezaji wa magari ili kupunguza msongamano nyakati za jioni na za asubuhi.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano, wengi wa wahudumu hao wakiongozwa na Elijah Mokua, msemaji wao, walisema kuwa barabara zinazoelekea kwenye steji kuu zinahitaji uelekezi wa maafisa wa trafiki kwani hutatiza mno hasa wakati gari zote huingia kwa steji hiyo.

Kulingana na wahudumu hao, hakuna uratibu unaofuatwa katika barabara inayotumiwa kuingiza gari zote kwenye steji hiyo iliyoko mkabala wa jengo la St Judes.

“Katika hii barabara ambayo tunahitumia kuingia kwa steji hatuelekezwi na afisa yeyote wa trafiki, na kila mwendesha gari hujitafutia njia au mbinu ya kumpenyesha kuingia,” alisema Godffrey Ochako, dereva mwingine.

“Tuko na barabara moja ya kuingia kwa steji hii inayopita eneo hili la St Judes, tunaomba uelekezi uwekwe eneo hilo ili maafisa wa polisi kutuelekeza jinsi ya kuingia kwa steji,” aliongezea Ochako.

Wakati huu ukarabati unaendelea katika steji ya magari yanayoenda Marani, Suneka, Nairobi, Manga, Nyamira, Itumbe na nyinginezo, huku wahudumu hao wakitaka ukarabati huo mpya kuharakishwa ili kuwapa nafuu wanapokuwa barabarani kwa shughuli za uchukuzi

“Lile ambalo tunaomba wahudumu wenzetu ambao ni waendesha pikipiki ni wawe na heshima kwetu maana mara nyingi hupita mbele yetu bila kuonyesha ishara yeyote na unaweza mgonga na ulaumiwe bure,” James Bosire, dereva mwingine alidai.