Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wenye magari na pikipiki wanaotumia barabara ya Chemelil/Muhoroni wamewaonya wafanyibiashara wanaouzia bidhaa zao barabarani.

Wahudumu hao wamesema wanalazimika kupunguza mwendo kupita kiasi na hata kulazimika kusimama wakati mwingine wanapofika katika soko la Apidi lililoko kwenye barabara hiyo.

Philip Ojwang' ni mmoja wa wahudumu wa matatu katika barabara hiyo aliyelalamikia vikali tabia hiyo akiwataka wanaoendesha biashara zao karibu sana na barabara kuheshimu sheria za trafiki na pia kujali usalama wao.

''Soko ni kubwa, kwa nini wakaribie hadi eneo la magari kupitia? Ajali itakapotokea kama kawaida maadamu ni sisi madereva tutakaolaumiwa,'' alisema Ojwang' mnamo siku ya Jumanne.

Aidha, wenye pikipiki nao wanasema kuwa wametatizika pakubwa kufuatia hali hiyo ambayo kwa sasa wanadai ni ya muda mrefu, na sasa wamewataka wafanyibiashara hao waheshimu sheria za barabara.

Wakazi katika eneo hilo ambao pia wanashuhudia jinsi hali ilivyo, wameitaka serikali ya Kaunti ya Kisumu kuwajengea wafanyibiashara hao soko maalumu ili kumaliza tatizo hilo.

Hali kwenye soko hilo huonekana ya kutatanisha, wakati hata magari ya kubeba yanaposimama barabara na wenyewe kuwauzia wateja bidhaa bila kujali hatari iliyoko.