Halmashauri ya uchukuzi na usalama wa barabarani nchini imewapa makataa ya mwezi mmoja wahudumu wa tuktuk na bodaboda katika ukanda wa Pwani kujiunga na vyama vya ushirika kabla ya kuchukukuliwa hatua.
Onyo hilo limetolewa na Afisa mkuu Mtendaji wa Halmashauri hiyo Sammy Mbura, aliyesema kwamba watakao kaidi agizo hilo watachukuliwa hatua za kisheria kwani hatua hiyo itawasaidia katika utekelezaji wa uchukuzi.
Akizungumza mjini Mombasa katika mkutano wa wadau hao siku ya Ijumaa, Mburu aliwatahadharisha wale wanaokiuka sheria za trafiki kuwa serikali itawaadhibu kwa mujibu wa sheria kwani wengi wao wamechangia ajali nyingi za barabara huku idadi kubwa ya vijana wakiaga dunia wangali bado wadogo.
“Ni lazima wahudumu wote wa tuktuk pamoja na bodaboada na hata wale wa magari ya uchukuzi wa umma kuzingatia sheria za barabarani ili kuepukana na ajali za mara kwa mara na kuokoa maisha ya abiria,” alisema Mbura.
Aidha, alisema kwamba maafisa wa trafiki na wale wa halmashauri hiyo watakuwa wakizunguka nyanjani na kuwachunguza wahudumu ambao bado hawajajiunga na vyama vya ushirika na kuwachukulia hatua za kisheria.
“Wale watakaopatikana bado hawajajiunga na vyama vya ushirika wataadhibiwa. Tafadhilini msidharau hivi vyama kwa sababu vitawasaidia katika kutatua mzozo na hata kuwasilisha lalama zenu katika halmashauri ya uchukuzi na usalama wa barabarani,” aliongeza Mbura.
Hatau hiyo imejiri huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 60 ya ajali za barabarani husababishwa na wahudumu wa tuktuk na bodaboda katika ukanda wa Pwani.