Waumini wa dini ya Kiislam mjini Mombasa wameungana na wenzao kote nchini katika kuadhimisha sikukuu ya Eid-al-Adha.
Akiwahutubia wafuasi wa dini hiyo katika uwanja wa Kaunti ya Mombasa mjini Mombasa siku ya Alhamsi, Kadhi mkuu Sheikh Sharrif Muhdhar aliwahimiza Waislamu kukumbatia amani na kuchangia katika kuhakikisha kwamba taifa hili lina usalama.
“Ni vyema iwapo Waislamu wataungana na kukumbatia amani sambamba na kudumisha uiano na utangamano na kupiga vita uhalifu ili taifa hili liwe na usalama,” alisema Sheikh Muhdhar.
Kadhi mkuu wa zamani nchini Sheikh Ahmed Kassim amewakosoa wale wanaolenga kuzua upinzani na mabishano ndani ya jamii ya Kiislamu kuhusiana na siku ya kufanyka kwa sherehe hiyo akisema kwamba Waislamu wanafaa kuungana na kuheshimu misingi ya dini hiyo.
“Kama Waislamu sio vyema kuzua upinzani na kuleta vurugu katika taifa letu lililosalama. Ningependa kila Muislamu kupenda mwenzake na kuwa katika mstari wa mbele kueneza amani na kujitenga na wale waliyo na malengo potovu ili kuvuruga usalama wetu,” alisema Sheikh Kassim.
Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Maimamu na wahubiri humu nchini CIPK katika kaunti ya Mombasa Sheikh Mahmoud Abdillah, aliwahimiza Waislamu kuungana na wale wasiyobahatika katika jamii katika kuadhimisha sikukuu hiyo na akawataka washerehekee kwa ungalifu na kuzingatia kutoa sadaka.
“Ningependa kuwahimiza Waislamu wote tuzingatie maagizo ya Quran katika kusheherekea kwetu ili tusiende kinyume na sheria za mwenyezi Mungu. Tuchinje kwa haki kwa kusherehea na wale wasiobahati na tuzidi kutoa sadaka,” alisema Sheikh Abdillah.
Sherehe za sikukuu hiyo ya Eid-al-Adhazinaashiria kukamilika kwa funga ya siku tisa katika ibada zinazoendelea katika Mji Mtukufu wa Makka baada ya kukamilika kwa sherehe za sikukuu ya Ramadhan.