Baadhi ya wakaazi wa Wadi ya Keumbu katika eneo Bunge la Nyaribari Chache wamepongeza Serikali ya Kaunti ya Kisii kwa kuinua viwango vya huduma katika hospitali ya Keumbu.
Wakiongea siku ya Ijumaa na Mwaandishi huyu katika hospitali ya Keumbu, wakaazi hao walimpongeza Gavana James Ongwae kwa kuinua viwango vya hospitali hiyo kwa maswala ya huduma haswa kwa kuwepo kwa mashine ya kutumika katika upasuaji ambayo ilibuniwa siku ya Ijumaa.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya Gavana Ongwae kutembelea hospitali hiyo na kuanzisha mradi huo.
"Napongeza Serikali ya Kaunti yetu ya Kisii kwa kutukumbuka na kutusaidia katika hospitali hii ili nasi tuweze kunufaika na huduma bora ya afya," alihoji Emily Biyaki mkazi.
Wakaazi hao walisema kuwa kutokana na kuongezwa kwa madktari wawili, sasa wana matumaini kuwa watasaidika pakubwa.
"Tumekuwa na shida kubwa kwa kuwa na daktari mmoja lakini kwa sasa hatuna shida hiyo tena kwani tumepata daktari wengine wawili," alihoji Daniel Mwancha, mkaazi mwingine.
Kwa mujibu wa wakaazi hao, kwa sasa watapata matibabu katika hospitali hiyo bila kuenda katika mji wa Kisii kutafuta matibabu kama hapo awali.