Waziri wa kilimo katika kaunti ya Kisii Vincent Sagwe, amewataka wakaazi wa kaunti hiyo kujitahadharisha dhidi ya watu ambao wamesemekana wanazunguka huku wakiwahadaa watu kuwa wanawapa kazi iwapo watalipa shilingi elfu mbili.
Waziri huyo akiongea siku ya Jumatano katika ofisi yake, alisema kuwa watu hao wanaendelea kufanyiwa uchunguzi ili kubainisha uhalali wa shughuli wanazojihusisha nazo.
“Nawaonya watu wote kuwa macho wanapoitishwa pesa na watu wasiowajua kwa madai ya kuwapa kazi. Ni kinyume na sheria kulipa pesa ili upate kazi," alisema Bwana Sagwe.
Pia aliwataka watu wote ambao wanataka kazi kupata ujumbe na habari za kuaminika kutoka ofisi yake na hasa ofisi ya mawasiliano amabyo ina habari zote za kaunti zinazo husiana na miradi yote inayotekelezwa na kaunti ya Kisii.
“Ofisi zetu za kaunti ziko wazi kila wakati kwa hivyo wakaazi sharti wafikiri mara mbili iwapo mtu anawaomba pesa ili awape kazi. Ni wazi kuwa mkurugenzi mzima hawezi kuomba mtu pesa ili ampe kazi,” alisema Sagwe.
Onyo hilo limetolewa siku mbili tu baada ya mtu mmoja ambaye anajifanya kuwa mkurugenzi mkuu wa shirika moja lisilo la kiserikali kuzunguka katika miji ya Kisii huku akiwatapeli wakaazi.
Aliwalaghai wakaazi kuwa anawapa kazi ya kuwaelimisha wakulima na wafugaji kuhusiana na ubora wa kuwalisha ng’ombe na mbuzi na ukuzaji wa mimea katika wilaya ya Gucha.