Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu gavana wa kaunti ya uasin Gishu Daniel Chemno ametoa onyo dhidi ya matumizi ya vyakula na maziwa ambayo hayajafanyiwa uchunguzi, akisema kuwa baadhi ya bidhaa hizo huchangia asilimia kubwa ya kusambaa kwa ugonjwa wa saratani.

Naibu huyo alisema kuwa wengi wa wakulima hawajui kuhifadhi vyakula kwa njia inayofaa, na hupelekea vyakula kupata viini vya Aflatoxin.

Chemno aliyasema haya katika kongamano la ‘HealthBlos Regional Cancer’ lililoandaliwa katika hoteli moja mjini Eldoret, na kuongezea kuwa takriban watu elfu thelathini na sita hupata maradhi ya saratani kila mwaka huku wengine zaidi ya elfu ishirini na sita wakipoteza maisha yao.

Kongamano hilo limeandaliwa na hospitali za Kimbilio Hospice, Hospitali ya rufaa na mafunzo ya Eldoret, Hospitali ya Mediheal na Reale, Chuo kikuu cha Nairobi na Kaunti ya Uasin Gishu ikijumuisha wakazi wa kaunti ya Uasin Gishu, Nandi, Trans Zoia, Elgeyo Marakwet, baringo, west Pokot na Turkana.

Naibu gavana huyo amekuwa katika msitari wa mbele kuhakikisha kuwa wakazi wa kaunti ya Uasin Gishu wanapata chakula na bidhaa bora, ikizingatiwa kuwa sekta ya afya ndiyo nguzo muhimu kwenye ukuaji wa uchumi.

Aidha, Chemno pia amewarai wakazi kutonunua bidhaa ambazo huenda ubora wake haujakaguliwa na Taasisi ya ubora wa bidhaa nchini KEBS.

Wito huu unatolewa siku chache baada ya hofu kuhusu viini hivyo vya Aflatoxin kuzuka nchini.