Wakazi wanaoishi katika vitongoji duni vya Moroto eneo la Tudor na Kalahari katika kaunti ya Mombasa wamedinda kuyahama makazi yao wakisema kwamba lazima serikali iwaonyeshe mahali maalum kwa kuenda kuishi.
Hii ni kutokana na tahadhari kutolewa na wanasayansi wa idara ya utabiri wa hali ya anga kuwa maeneo ya vitongoji duni na yale ya mabonde huenda yakashuhudia mvua kubwa zaidi na kusababisha maporomoko ya ardhi katika makazi yao.
Wakiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, wakazi hao wakiongozwa na mzeeGilbert Mwai walisema kwamba waliishi katika makaazi hayo kwa muda wa miaka zaidi ya kumi, na iwapo serikali inajali hali yao ya kiafya na kimazingira, basi ingefaa kuwaelekeza mahali kuenda kuishi badala ya kuwaambia wayahame makazi yao pasi na kujua pa kwendaishi.
“Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba serikali pamoja na viongozi wa kisiasa kutuambia tuhame makazi yetu ilhali hawajatuambia pahali pa kuishi, sasa tuhame twende wapi, kwani wanatuambia tutaweza kujenga nyumba zetu ama tutaishi tu kwa mahema,” alisema Mwai, mzazi wa watoto saba.
Aidha, alipendekeza serikali kubuni mbinu mbadala za kuzuia mafuriko na maporomoko katika maeneo ya makazi yao ili kuepukana na maafa endapo yatatokea kwani baadhi ya wakazi wanahofikia kuwa huenda baadhi ya mabwenyenye wanatumia fursa hiyo kunyakua ardhi zao.
“Sisi hatuoni tukihama makazi yetu ya toka enzi za babu zetu kwa sababu ya mvua ya Elnino, hiyo itakuja na itaenda. Tunapendekeza serikali kuu na ile ya kaunti ya Mombasa kubuni mbinu mbadala za kuzuia athari za mvua hiyo kwa sababu tunahofia huenda watu flani wakatumia fursa hiyo kunyakua ardhi zetu,” aliongeza Mwai.
Mvua hiyo ya Elnino inayokisiwa kupanda hadi viwango vya mililita 250 katika kauti ya Mombasa na eneo zima la pwani huenda ikasababisha madhara makubwa pamoja na uharabifu wa mazingira.