Share news tips with us here at Hivisasa

Chifu wa kata la Kesses Bi Sally Letting amewaonya wakazi wa eneo hilo dhidi ya utengenezaji wa pombe haramu huku akitoa onyo kali kwa watakaopatikana wakiendeleza biashara hiyo.

Akizungumza katika eneo la Kesses katika mazishi ya Bi Mary Birgen siku ya Jumanne, chifu huyo alisema kuwa wataendelea kuchunguza wanakijiji wanaoshukiwa kuendesha biashara hiyo kisiri.

“Nafurahia kuwa tumeweza kunasa baadhi ya watu wanaotengeneza pombe hiyo haramu kijijini. Hatutachoka katika vita hii na iwapo yeyote atapatikana, basi atachukuliwa hatua kali ya kishiria ikiwemo kulipa faini kubwa,” alisema Letting.

Chifu huyo vilevile amewaomba wanakijiji kusaidiana nao kutafuta wanaoendesha biashara hiyo huku akitaka wazazi kutekeleza wajibu wao wa kuwa mfano bora kwa wanao.

“Kila mzazi ana jukumu la kulea wanao vyema. Inasikitisha kuwa baadhi ya wazazi wanaotengeneza pombe haramu wanahusisha wanao kwenye biashara hiyo,” aliongeza chifu huyo.

Bi Letting pia amewahimiza wanaotengeneza pombe hiyo kutumia mitungi za kuhifadhi pombe kuteka maji ya mvua ya El Nino ambayo imeanza kushudiwa katika eneo hilo, siku mbili zilizopita.