Wakazi Kitutu Chache Kaskazini wamelalamikia ongezeko la bei ya mahindi katika eneo hilo na kuhofia kuathirika na makali ya njaa.
Wakizungumza Jumatatu katika soko la Marani, Eunice Moseti na Irene Kwamboka walisema kuwa kufuatia ongezeko la bei ya mahindi, huenda wakabiliwe na njaa kwa muda mrefu kwani bei ya mahindi imeongezeka kupita kiasi.
Hii ni baada ya mahindi kutofanya vyema katika maeneo mbalimbali ya Kisii na kupelekea kupanda kwa bei ya mahindi mara dufu.
Aidha, wakazi hao waliomba serikali kuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti kuleta mahindi humu nchini kutoka nje ya nchi kama njia moja ya kukabiliana na njaa ambayo imenukia katika maeneo hayo ya Kisii.
Wengi wa wakazi hao wamesema walikuwa wakinunua mahindi mkebe wa kilo mbili kwa shillingi 50 lakini bei hiyo imeongezeka hadi shillingi 90.
“Tunaomba serikali ya kitaifa kuleta mahindi kutoka nje ya nchi kuhakikisha wananchi hawatakabiliwa na njaa kamwe. Serikali ikifanya hivyo hatutakuwa na la kuogopa,” alisema Mary Onsongo ambaye ni mkazi.