Wakazi pamoja na wafanyibiashara katika kaunti ya Kisii wameombwa kuimarisha usafi na kujiepusha na kutupa uchafu kiholela.
Akiongea siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa jumuia moja ya vijana ya kuzoa taka, 'The Green Youth', Samoita Maina alisema kuwa wakazi wa mji wa Kisii wamekuwa na mtindo wa kuamka asubuhi na kutupa taka njiani bila kuzingatia usalama na hatari za kiafya.
Maina alisema kuwa baadhi ya vijana wa mtaa wamekuwa wakilipwa na wakazi kubeba taka na badala ya kuipeleka mahali pafaao wanaitupa njiani hali ambayo alisema huenda ikasababisha mkurupuko wa maradhi.
“Serikali ya kaunti ya Kisii inapaswa kutafuta mbinu ya kuwashika wakazi ambao wana mazoea ya kutupa taka kila mahali,” alisema Maina.
Baadhi ya wakazi wa eneo la KARI liloko viungani mwa mji wa Kisii, walisema kuwa wanafanya hivyo kwa kukosa vifaa vya kuwekea uchafu na taka zinazotoka kwenye maeneo ya makazi.
Bi Jane Ondimu, ambaye huuza mboga katika eneo hilo, alisema kuwa yeye hukusanya uchafu na kuwapa watu wa kaunti ambao hukusanya taka hiyo.
Hata hivyo, aliiomba serikali ya kaunti kuangalia suala hilo na kutenga vituo maalumu vya kuweka taka hiyo.
James Magaki, ambaye ni mmliki wa nyumba katika eneo la Jogoo, alisema kuwa sharti wakazi hasa wenye nyumba waeke mikakati ya kuhakikisha kuwa taka hazitupwi popote.
Alisema wakazi wanapaswa kutenga mahali maalumu pa kuweka taka kabla ya kuzolewa na wafanyikazi wa serikali ya kaunti.