Wakazi Kisii wametakiwa kujiepusha na kujikinga mvua chini ya miti wakati wa mvua ya El Nino ambayo inatarajiwa kuanza mwezi wa Octoba na kuendelea hadi mwaka ujao wa 2016.
Akiongea kwenye afisi yake siku ya Jumatano na mwandishi huyu, mkurugenzi wa idara ya hali ya anga, Henry Sese, alisema sharti wakazi wawe makini na kuhakikisha kuwa wanao wako mahali salama wakati wa mvua.
Alisema huenda kukashuhudiwa hali ya mumweko ambayo husababisha radi, ambazo mkurugenzi huyo alisema zinaweza kusababisha maafa iwapo watu watakuwa wanajikinga chini ya miti.
Aidha, mkurugenzi huyo aliongeza kuwa watu sharti wajiepushe na maeneo tambarare kwa sababu maeneo kama hayo huathiriwa na radi.
“Ni vyema watu wafahamu kuwa wakiona mawingu ni ishara kuwa mvua ipo karibu hivyo basi wahakikishe wanaenda nyumbani au mahali ambapo wanaweza kujizuia mvua, lakini isiwe karibu na miti au maeneo ya tambarare, kwani wanaweza kupigwa na radi na kuaga dunia,” alisema Bwana Sese.
Mkurugenzi huyo aliwaomba viongozi ambao wanajukumika katika uongozi wa vijiji na miji kusambaza ujumbe huo kwa watu wote ili jamii iweze kumakinika na kuepushwa na maafa ambayo huenda yakaletwa na mvua ya El Nino.