Watu wanaokaa eneo la Kona ya Zamani Likoni wameitaka serikali ya kaunti kwa kushirikiana na serikali kuu kuwapa neti kuzuia mbu.
Pia, wakazi hao wanataka serikali kuwatafutia njia ya kuwaepusha na maafa ambayo yanatarajiwa kuletwa na mvua ya El Nino mwezi ujao.
wakazi hao ambao walioongea Jumamosi walisema kuwa serikali haijakuwa ikiwashughulikia kila mara kunapotokea mafuriko. Hii ni ikizingatiwa kuwa eneo hilo huathirika mno nyakati za mvua kubwa kwa sababu ya kuwa tambarare.
Walisema wanahofia kupoteza mali yao iwapo serikali haitachukua hatua kuwaelekeza na kuweka mipango ya dharura kudhibiti hali.
Mzee Ramadhan Mumbo, ambaye ni mzee wa mtaa katika sehemu hiyo alisema kuwa wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakimletea lalama zao wasipatikane bila mipango.
Mumbo alisema mara nyingi eneo hilo mbali na kwamba liko tambarare, huwa na mashimo mengi ambayo hujazwa maji ya mvua na huwa timbo la kuzaliana mbu.
Wakazi wanahofia huenda kukazuka malaria na ndio kuitaka wizara ya afya kuwa mstari wa mbele kuzuia maafa hayo.
Pia alitoa wito kwenye mashirika ya masuala ya afya ya kijamii kutembelea maeneo hayo na kuwapa msaada wa ushauri wa kiafya na masuala mengine ambayo yanahusiana na mvua hiyo.