Wakazi wa eneo la Miritini katika Kaunti ya Mombasa wamelalamikia kucheleweshwa kwa malipo yao ya fidia kutoka serikali ya taifa kwenye mradi wa kutengenezwa reli ya kisasa ya SGR.
Wakazi wengi kutoka kaunti za Mombasa, Kilifi pamoja na Taita Taveta, ambao waliweza kuathirika na mradi huo wameshafidiwa lakini baadhi yao bado wanangoja fidia zao.
Joseph Thoya mkazi wa Miritini ambaye aliongea siku ya Alhamisi kwa niaba ya waathiriwa 40 kutoka eneo hilo, alisema kuwa waliambiwa wangoje kufika mwezi jana na pindi mwezi huo ulipowadia walitakiwa tena kuwasilisha majina yao upya kwenye mamlaka husika, ambapo walifanya walivyotakiwa.
Thoya alisema mpaka sasa zaidi ya mwezi umepita tangu wawasilishe majina yao lakini bado hawajaona kitu.
Wakazi hao kupitia msemaji huyo wao walishangaa ni kwa nini hela hizo zimepokezwa wengine na wao bado hawajapewa pesa zao ilhali eneo hilo ni moja kati ya yale yaliyotiwa alama mapema.
“Tunaiomba serikali ya taifa kufanya hisani na kutupa fidia ndipo tuweze kujiendeleza kwa kuanza miradi ya kilimo au biashara ili angaa tulishe familia zetu,” alisema Thoya.
Mradi huo ambao tayari umeanza kwenye awamu za mwanzo, ni kati ya miradi mojawapo ambayo inalenga kuboresha uchukuzi wa bidhaa kutoka bandari ya Mombasa, hadi sehemu nyingine za nje na nchi nyingine jirani.