Wakazi wa Mombasa wameshinikizwa kuzingatia tahadhari zilizotolewa na Idara ya utabiri wa hali ya anga nchini kuhusu athari ambazo huenda zikashuhudiwa wakati wa mvua ya El Nino.
Kulingana na aliyekuwa Meya wa Baraza la mji wa Mombasa Sharrif Shekue, iwapo wakazi pamoja na viongozi wa Kaunti ya Mombasa watapuuza tahadhari hiyo, basi huenda athari za mafuriko zikashuhudiwa.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne katika kikao cha mazingira, Shekue alisema kwmaba ni jukumu la Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya kimazingira na wataalam wa El Nino kuweka mikakati mwafaka ya kudhibiti athari iwapo zitatokea.
Aidha, alipendekeza serikali ya kaunti ya Mombasa kutumia fedha wanazokusanya za ushuru kurekebisha mabomba ya maji taka na mitaro ili kuzuia kushuhudiwa madhara ya kiafya pamoja na nyumba za wakazi kuanguka.
“Itakuwa vyema iwapo serikali ya Kaunti ya Mombasa itashirikiana na wadau wa kimazingira ili kuona kwamba madhara ya kiafya yanadhibitiwa. Mabombo ya maji taka pia yanafaa kurekebisha. Bila kuzingatia hilo, basi huenda kukashuhudiwa nyumba za wakazi kubomoka,” alisema Shekue.
Shekue aliitaka serikali hiyo ya kaunti kuwatuma masorovea kukagua maeneo ambayo huenda yakaathiri zaidi na mvua hiyo na ukarabati wa mabomba ya maji taka na mitaro kuanza kushughulikiwa kwa wakati mwafaka.
“Tunaomba serikali ya kaunti pia watume masorovea kukagua sehemu ambazo zinakisiwa huenda zikaathirika na mvua hiyo, ama wakazi washikizwe kuyahame maeneo hayo na watengewe maeneo mazuri watakayohamia,” aliongeza Shekue.
Mvua hiyo ya El Nino inatarajiwa kuanza kushuhudiwa kote nchini wakati wowote mwezi huu wa Oktoba hadi Januari mwaka ujao.