Wakazi kutoka Kaunti ya Mombasa wametakiwa kusaidia kutoa ripoti dhidi ya magenge ya watu wanaozunguka na kujifanya maafisa wa polisi na kuwahangaisha watu kwa kuwanyanganya mali yao na kuwapiga.
Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Jumatatu, katika ofisi yake, kamishna wa kaunti ya Mombasa, Nelson Marwa alisema kuwa watu hao ambao wanaaminika kutembea nyakati za usiku hasa katika mitaa mbali mbali ya mji huo, ikiwemo Majengo, Old Town, pamoja na kisiwani, wamekuwa wakienda katika maskani ya watu wakati wa usiku na kudai kuwa polisi na pindi mhusika anapofungua mlango, wanamshambulia na kumibia mali yake.
Marwa alisema kuwa msako na doria dhidi ya genge hilo umeanza kwenye mitaa yote mjini Mombasa ili kuwakamata wahalifu hao na kuwachukulia hatua ya kisheria.
Kamishna huyo aliwataka wakazi kutoa ripoti dhidi ya watu ambao wanawashuku kuwa na vitendo kinyume na sheria katika mitaa yao.
Aidha, Marwa alikemia vikali kundi moja la viajana ambalo linajiita Mombasa CrimeAlert ambalo alilishuku kuwa huenda ndilo limehusika katika mashambulizi ya hivi karibu yaliyofanywa dhidi ya wakazi.
Kisa cha hivi karibuni kikiwa kushambuliwa kwa afisaa wa polisi na kuuliwa na kupigwa kwa wakazi kwenye mitaa ya Majengo na Old Town.
“Iwapo utagongewa mlango na mtu ambaye anajitambulisha kama polisi, usifungue wala usiongee. Watu hao ni wahalifu ambao wanajifanya polisi, na ukiwa na ripoti ya watu ambao unawashuku kujihusisha katika uhalifu, piga ripoti kwenye idara ya polisi,” alisema Marwa.
Aliahidi kupigana na uhalifu kwenye kaunti hiyo hadi magenge haramu yaangamizwe kabisa.