Wakazi kutoka eneo la Mtongwe, mjini Mombasa wamelalamikia ukosefu wa usalama katika mtaa huo na kuitaka idara ya polisi kuimarisha doria zao hasa katika nyakati za asubuhi na jioni.
Wakazi hao walisimulia jinsi ambavyo wamekuwa wakishambuliwa wakati wa asubuhi wanapoenda kazini na jioni wakirudi kutoka shughuli zao, ambapo walisema wao hupigwa na kunyang’anywa pesa, simu pamoja na vitu vingine.
Mzee Jamal Lule, ambaye ni mshirikishi wa usalama na uongozi wa Nyumba Kumi katika eneo la Vijiweni katika mtaa huo wa Mtongwe, alisema kuwa lawama nyingi zinawaangukia maafisa wa usalama ambao alisema kwa mara nyingi wamekuwa tu wakionekana wakati wa msako wa kutafuta walanguzi ilhali usalama unahitajika kuhakikishiwa wakazi wakati wowote ule.
“Usalama wa maeneo yote katika mtaa huu umedorora kwa sababu ya ukosefu wa kazi miongoni mwa vijana ambao hunyakua visivyo vyao kutoka kwa wakazi,” alisema Lule.
Alikitaja kisa ambacho watu zaidi ya kumi walishambuliwa kwa visu na marungu na wahalifu wiki jana walipokuwa wakielekea kazini katika eneo la KD, mojawapo ya njia ambayo wakazi hutumia kimkato kuelekea eneo la kivuko cha Likoni ili kuvushwa kuelekea kisiwani Mombasa.
Aliitaka idara ya usalama kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Mombasa kuwaletea kituo cha polisi karibu ili vijana hao ambao wanaendelea kuongezeka na kuweka maisha ya wakazi hatarini wakamatwe.