Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi wa Kaunti ya Nakuru wametakiwa kujilaumu wenyewe kwa kukosa kushiriki katika vikao vinavyoitishwa ili kuthamini mapendekezo na makadirio yaliyo kwenye bajeti.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano mjini Nakuru, mwakilishi wa wadi ya Kaptembwa, Daniel Ambale alisema kutoshiriki katika mikutano hiyo kuna hatari kwani mapendekezo ya wananchi huenda yakakosa kuzingatiwa na serikali iliyoko mamlakani.

Ambale alisema kwamba hatua hiyo inailazimu serikali iliyo mamlakani kupitisha mapendekezo yake, ambayo wakati mwengine huwa hayaambatani na matakwa ya wananchi.

“Hali ya umaskini na hali ngumu ya maisha ndiyo sababu kuu ya wananchi kutojihusisha katika mikutano hiyo,” alisema Ambale.

Aidha, mwakilishi huyo, ambaye pia ni kiongozi wa waliyo wachache katika bunge la Kaunti ya Nakuru, alisema kuwa ni muhimu wakazi wa Kaunti ya Nakuru wazingatie ulipaji wa ushuru pasi na kufeli ili kuongeza ushuru unaokusanywa kwa sasa na kaunti hiyo wa takriban Sh2.5bn.

Hata hivyo, Ambale aliwaomba wakazi wa kaunti ya Nakuru na wananchi kwa ujumla, kujitokeza na kujihusisha kwa kutoa maoni yao punde wanapohitajika kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba, kwa mustakabali wao.