Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Bi Josphine Onunga amewaomba wananchi kutia bidii katika shughuli zao za kila siku ili kusaidia kaunti hiyo kuangamiza umaskini.

Akizungumza siku ya Jumanne kwenye hafla yakusherehekea siku ya mashujaa nchini, kwenye uga wa michezo ya Nyamaiya, Onunga alisema kuwa umaskini nchini unaweza ukaangamizwa iwapo wananchi watajitolea kufanya kazi kwa bidii ili kujistawisha kimaendeleo.

"Viwango vya juu vya umaskini kwenye taifa hili hasa huku Nyamira vinaweza kuangamizwa iwapo wananchi watajitolea kufanya kazi kwa bidii ili wajistawishe kiuchumi,” alisema Onunga.

Kamishna huyo alisema kuwa anatarajia kwamba Kaunti ya Nyamira imo mbioni kuhakikisha kuwa inafanya shughuli zakujiendeleza kwa saa 24 kwa siku ili kuimarisha uchumi wake.

"Ninatumai kuwa Kaunti ya Nyamira itaanza kufanya shughuli zakuimarisha uchumi wake kwa saa ishirini na nne kwa siku na hili litaafikiwa baada yetu kudhibiti visa vya ukosefu wa usalama miongoni mwa wananchi,” alisema Onunga.

Kamishna huyo aidha alisema kwamba swala la ugemaji na unywaji wa pombe haramu kwenye kaunti ya Nyamira lingali bado donda sugu.

"Ugemaji na unywaji wa pombe haramu ni changamoto ambayo tunazidi kukumbana nayo humu Nyamira. Nawaomba wananchi kuepukana na tabia hizo kwa kuzingatia masomo, hasa ya wasichana ili kusaidia jamii kujistawisha zaidi,” aliongezea Onunga.

Akizungumzia swala la ukeketaji wa wasichana, Onunga alisema kuwa tamaduni hiyo kamwe haitoruhusiwa na serikali huku akisema yeyote atakaye patikana akitekeleza ukeketaji atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, Onunga aliwasihi wananchi kutopuuza onyo la mvua ya El Nino akisema kuwa lazima wananchi wawe macho mvua hiyo inapoanza kunyesha kwenye maeneo mengi nchini.