Wakazi wa eneo bunge la Borabu kaunti ya Nyamira wamempongeza Wakili Alfaxard Osoro kwa kuwachimbia visima vya maji katika wadi zote za eneo bunge hilo.
Wakizungumza siku ya Alhamisi wakati Osoro alikuwa anafungua rasmi miradi hiyo ya maji katika eneo la Riamasara Nyasiongo, wakazi hao walimpongeza wakili huyo kwa kuwaletea maji karibu na kwao.
“Tumekuwa tukisumbuka sana haswa kwa sekta ya maji maana tuliwachagua viongonzi lakini hakuna aliyejitolea kutuchimbia visima katika eneo hili. Tunampongeza wakili Osoro na tunamuomba aendelee na usaidizi huo aliyo nayo,” alidokeza Mary Osinyo, mkazi.
Wakili huyo alifungua miradi hiyo ya maji katika eneo la Kiabonyoru, Mekenene, Mongori na Riamasara huku akisema ataendelea kuwasaidia watu wa eneo hilo vile awezalo.
“Niliona mkisumbuka sana katika eneo hili haswa kwa sekta ya maji na nimejaribu nikachimba visima katika kila wadi za eneo hili. Nafungua miradi hii ya maji haya rasmi ili muanze kuyatumia,” alisema Osoro.
Eneo bunge la Borabu lina wadi nne na kila wadi ilinufaika kutokana na mradi huo wa maji.
Wakili huyo aliwaomba vijana wote wa eneo hilo kuwajibika katika kufanya kilimo kuliko kutegemea kazi za ajira ambazo hazipatikani kwa urahisi.
“Naomba vijana wote wafanye kazi ya kilimo pamoja na biashara ili kujiendeleza kimaisha badala ya kukaa wakingoja kuajiriwa katika ofisi,” alisema Osoro.