Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Zaidi ya wakazi 3,000 kutoka mitaa ya mabanda ya Dunga Unuse na Mbuyuni eneo bunge la Changamwe, wameapa kutoondoka kwa ardhi hizo.

Wakizungumza siku ya Jumanne wakati wa mkutano katika mtaa wa Dunga Unuse uliohudhuriwa na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi, wakazi hao waliapa kusimama kidete na kukataa jaribio la kuwafurusha kutoka ardhi hiyo ambayo imekuwa ikizozaniwa kwa muda mrefu.

Asha Nyambura, mkazi, alidai mzozo wa ardhi katika eneo hilo unaendelezwa na mabwanyenye wanaoitaka sehemu hiyo ili kujinufaisha wenyewe.

Hata hivyo, mkuu wa idara ya Ardhi na mipangilio katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya, aliwahakikishia wakazi hao kuwa watawaunga mkono kwa dhati huku akiwataka wakazi hao kuungana kutetea ardhi yao.

Thoya alikanusha madai kuwa ardhi ya Dunga Unuse na Mbuyuni ni za umma na kuwa kuna miradi inayotarajiwa kuanzishwa katika maeneo hayo.

“Sijachochea wakazi kupinga miradi inayotarajiwa kutekelezwa na serikali katika eneo hili, ila serikali inahitaji kutoa makubaliano na malipo mazuri kwa wenyeji wa eneo hili,” alisema Thoya.

Thoya aliwataka wakazi wa eneo hilo kutokubali kugawanywa kwa misingi ya kidini wala kikabila na baadhi ya mabwanyenye wanayoikodolea macho ardhi hiyo iliyo mita chache kutoka bandari ya Mombasa.