Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi katika eneo bunge la Jomvu wanaitaka serikali ya kaunti kwa ushirikiano na serikali kuu kuwapa hati za umiliki za ardhi ili kuwaepusha kutoka kufurushwa na kubomolewa makazi yao kama ilivyoshuhudiwa hivi majuzi katika mtaa wa Dunga Unuse.

Wakazi hao ambao waliongea na mwanahabari huyu siku ya Jumapili, wakiongozwa na msemaji Simon Lule, walisema kuwa mabwanyenye wameanza kuwa na mtindo wa kulenga eneo hilo, baada yao kubaini kuwa wengi wa wakazi katika eneo hilo hawana stakabadhi rasmi za umiliki wa ardhi.

Lule alihofia kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za haraka kuwapa stakabadhi hizo, matapeli hao, ambao inadaiwa wanashirikiana na baadhi ya wanasiasa na wafanyabiashara mashuhuri kutoka mji wa Mombasa huenda wakanyakua ardhi yote na si tu Jomvu tu.

Msemaji huyo aliongeza kuwa kuna watu flani wamedaiwa kuzuru maeneo mbali mbali katika eneo bunge hilo ambao nia yao inashukiwa kuwa ya kupiga mnada ardhi ya sehemu hiyo, na kutaka wizara ya ardhi kulipa suala hilo dharura inayostahili.

Aidha, aliongezea kuwa wengi wa wakazi katika eneo hilo wamekuwa wakilala na wasiwasi kwa kuhofia kubomolewa nyumba zao usiku na wanyakuzi hao haramu wa mashamba.

Hata hivyo, kutokana na ziara ya waziri wa ardhi katika kaunti ya Mombasa huenda ikazaa matunda iwapo atatekeleza ahadi aliyotoa kwa wakazi kuwa kaunti itaharakisha uchunguzi wa suala hilo, na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika ambao walihusika kubomoa na kuwafurusha wakazi kwenye mtaa wa Dunga Unuse wiki jana.