Share news tips with us here at Hivisasa

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kisii, Mary Otara amewapa changamoto viongozi na wakazi kutoka kaunti hiyo kuwapa watoto wa kike kipaumbele katika masuala ya elimu.

Akiongea katika shule ya msingi ya Ibeno COG siku ya Jumatatu kwenye hafla ya kujadili masuala yanayowaathiri watoto wa kike, Otara aliwashauri waliohudhuria hafla hiyo kuzingatia masomo na kujiepusha na mienendo mibaya itakayo wapotosha maishani.

Otara pia alishtumu wale wazazi ambao wamekuwa na mazoea ya kuwaoza watoto wao kabla ya kumaliza masomo yao ya kidato cha nne huku akiwataka wakazi na jamii kwa jumla kutoa ripoti kuhusiana na yeyote ambaye atapatikana akiendeleza uhuni huo ambao alisema umepitwa na wakati.

Watoto wa kike ambao walihudhuria hafla hiyo waliweza kupewa sodo za hedhi, ambapo mwakilishi huyo aliahidi kuendelea kupigania haki za watoto wa kike pamoja na haki za jamii nzima ya gusii ili kujiendeleza kielimu.

“Nawaomba watu wote mlio hapa tushikane mikono ili kuhakikisha kuwa jamii yetu itainuka hasa mtoto wa kike, kwasababu bila mama hakuna jamii itakayoendelea. Viongozi wote ambao mnapigania haki ya watoto waendelee kufanya hivyo,” alisema Otara.