Hisia mseto zimetolewa na wakaazi wa eneo la Maseno kwenye kaunti ya Kisumu kufuatia madai ya mrengo pinzani wa Cord kutaka kuchangisha pesa za kuwalipa walimu ambao wako katika mgomo.
Wakaazi waliozungumza na huyu mwanahabari walisema kuwa jambo la kuchangisha pesa kutoka kwa wananchi si nzuri kwa kuwa litaonyesha kuwa serikali imeshindwa kufanya kazi yake.
"Cord haiwezi kuchangisha shilingi bilioni kumi na saba kila mwaka za kuwalipa walimu," alisema Monicah Odaro.
Doreen Asoka, mkaazi wa kijiji cha Sunrise alisema kuwa shughuli hiyo nzima ni njama ya CORD kujitafutia umaarufu, na huenda wakajizolea fedha nyingi kutoka kwa wakenya kwa manufaa yao wenyewe.
Hata hivyo, Asoka alishikilia kuwa ni lazima walimu walipwe nyongeza yao ya kati ya asilimia 50-60 kama ilivyoagizwa na mahakama ya kiviwanda ikiwa serikali inajiheshimu na inaheshimu mahakama.
"Hata rais mwenyewe alipitia mikononi mwa walimu, kwa hivyo si vizuri awapuuze jinsi anavyofanya," alisema Asoka.
Hata hivyo, wengine walisema kuwa mpango huo huenda ukafaulu kwa kuwa serikali imeshindwa kutimiza nyongeza hiyo.
"Mwezi mzima sasa umeisha bila ya watoto wetu kusoma. Hii inamaanisha kuwa serikali imeshindwa kuwalipa walimu na basi ni vizuri tuchange wenyewe," alisema Lawi Nabutete.
"Watoto wangu wawili wako nyumbani, na nahofia hata wanaweza kusahau waliyoyasoma mbeleni," aliongeza.
Lawi alisema kuwa yuko tayari kuchanga hela hizo iwapo ndiyo njia pekee a kuwakwamua wanafunzi kwenye tatizo la mgomo.
Pia, wakaazi hao wamesema kuwa jambo hilo ni aibu kwa serikali, na hivyo litawashurutisha wakuu wa serikali kuwapa walimu nyongeza hiyo.