Mradi wa maji wa takriban shillingi millioni tatu uliopendekezwa kuezekwa katika wadi ya Mekenene huenda ukasitishwa kutokana na kutokubaliana kwa wakazi wa vijiji viwili kuhusiana na sehemu pa kufanyika mradi huo.
Hii ni baada ya mkutano uliofanywa siku ya Jumatano kuamua mahali pa kuezekwa mradi huo kusambaratika pale ambapo wakazi wa vijiji hivyo viwili waliamua kuzozana.
Akiongea baada ya mkutano huo kusambaratika, mwakilishi wa wadi ya Mekenene John Ngeresa aliwasihi wazee wa vijiji hivyo viwili kufanya mkutano wa haraka na kuamua sehemu itakakayotengewa mradi huo wa mamillioni ya pesa au waupoteze.
"Nawakilisha vijiji vyote viwili, na nikichagua mahali patakapofanyikia mradi huo huenda nikaonekana kuonea pande moja na ndio maana nawasihi wazee wa vijiji hivyo kufanya mkutano na kuamua mahali pazuri pa kuezekwa mradi huo, na kama hilo halitofanyika, basi huenda mkapoteza mradi huo kwenda wadi nyingine," alisema Ngeresa.
Ngeresa aidha alishtumu malumbano hayo ila akasema kwamba hayafai kuwatenganisha wakazi wa vijiji hivyo viwili kwa kuwa serikali ya kaunti inayofadhili mradi huo itahakikisha kwamba usambazaji wa maji hayo kwa njia ya mifereji unawafikia wakazi wote sehemu hiyo.
"Sidhani kwamba sehemu pa kuezekwa mradi huo ni swala linalofaa kutuletea shida kwa kuwa nina hakika serikali ya kaunti itasambaza maji hayo kwa njia ya mifereji hadi kwenye soko mbalimbali na shule huku Borabu," alisema Ngeresa.
Mwakilishi huyo aidha aliwapa wiki mbili wazee wa vijiji hivyo kuamua eneo la kufanyikia mradi huo na kisha kuwasilisha mapendekezo yao mbele ya kamati inayosimamia mradi huo.
"Nimewapa wazee wa vijiji husika wiki mbili tu kuamua hatma ya mradi huu na kisha baadaye kuwasilisha mapendekezo yao mbele ya kamati inayosimamia mradi huo wa maji ili hatua kuchukuliwa," alihoji Ngeresa.
Mradi huo unafadhiliwa na halmashauri ya huduma za maji la Ziwa Victoria na serikali ya kaunti ya Nyamira.