Wakazi wa kaunti ya Nyamira wameomba viongonzi na wanasiasa wa kaunti hiyo kuandaa mkutano ili kutafuta suluhu ya mikasa ya moto katika shule za Nyamira.
Hii ni baada ya shule ya upili ya Nyakongo, Kaunti ya Nyamira kuchomeka siku ya Jumapili usiku huku bweni la wanafunzi 71 kuteketea na kuwalazimu wanafunzi hao kukesha usiku kucha kwa kukosa mahala pa kulala.
Wakiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Nyamira, wakaazi hao walisema ili mikasa ya moto kutafutiwa suluhu katika shule zote za Nyamira, sharti sekta ya elimu, wanasiasa na viongonzi kutoka kaunti nzima ya Nyamira kuwa na mkutano ili kutafuta suluhisho ya kuzuia mikasa ya moto ambayo inaendelea kushuhudiwa katika shule mbali mbali za kaunti hiyo.
"Umoja kati ya wahusika wote wa shule na ushirikiano kati yao na wanasiasa itakuwa njia mojawapo ya kuzuia mikasa baada ya kuweka mikakati kabambe kati yao," alisema Shem Bosire, mkaazi.
Wakati huo huo, wakazi hao pia walisema kuwa mikasa inapotokea uchunguzi unastahili kuanzishwa ili kubaini chanzo cha moto huo. Walisema kuwa ni muhimu sana kuwajulisha watu chanzo cha mikasa kama hiyo ili iwe rahisi kutafuta suluhu mikasa ya aina hiyo inapotokea.
“Mikasa ya moto inapotokea katika shule zetu suluhu ni kuandaa mkutano kati ya viongonzi, wanasiasa na wakuu wa elimu ili jibu halisi litafutwe kwa kuandaa kikao maalumu kutafuta jibu la mkasa ya moto," alisema Douglas Nyagaka, mkazi.
Mikasa ya moto imeathiri baadhi ya shule zilizoko kaunti ya Nyamira huku Shule ya upili ya Nyamaiya ikiwa mojawapo ya shule za wavulana za Nyamira zilitochomeka wiki jana.
Gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama alisema uchungunzi uanzishwe kubaini chanzo cha mikasa ya moto hiyo katika shule za Nyamira.