Wakazi kutoka wilaya ya marani katika kaunti ya Kisii wametakiwa kuacha kutumia pesa za watoto mayatima vibaya, na kuonywa kuwa sheria itawaandama iwapo watapatikana wakitumia hela hizo.
Kulingana na afisaa wa watoto katika eneo hilo, pesa ambazo watoto mayatima hupokea kila baada ya miezi miwili ni spesheli kwa matumizi ya mahitaji ya watoto hao kwa kujiendeleza katika masuala yao kimaisha.
Akiongea katika shule ya upili ya Igonga siku ya Alhamisi katika hafla inayoendelea ya kuwasajili watoto mayatima afisa wa watoto Judith Obutu alisema kuwa kuna badhi ya walezi na wasimamizi wa mayatima katika eneo hilo ambao wamekuwa wakichukua pesa hizo kwa niaba ya watoto hao, lakini baadaye huzitumia pesa hizo kwa masuala ambayo ni binafsi bila kuwapa watoto hao.
Alitoa wito kwa machifu na manaibu wao kutoa ripoti kwenye ofisi yake iwapo watakumbana na visa kama hivyo vya kutumiwa pesa za mayatima vibaya, na pia kuwashauri walezi hao pamoja na nyumba za kuwalea watoto hao kufuata utaratibu ambao unakubalika kisheria wanapochukua pesa hizo.
Aliwataka wakazi wa eneo hilo na eneo bunge hilo la Bonchari kuwaleta watoto mayatima katika vituo vya kuwasajili kwenye maeneo ya umma kama shule na vituo vingine ili waweze kuwekwa katika mpango huo wa serikali wa kupata shilingi elfu mbili kila mwezi ambazo hujumuishwa kwa miezi miwili na kupokezwa mayatima hao.