Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Shirika la Msalaba Mwekundu katika Kaunti ya Mombasa imewatahadharisha wakazi wa kaunti hiyo kuyahama maeneo ya mabonde ili kuepukana na mafuruko ambayo huenda yakashuhudiwa kutokana na mvua ya El nino inayotarajiwa kunyesha.

Kulingana na meneja wa shirika hilo katika Kaunti ya Mombasa Soud Tenga, huenda mvua hiyo inayotarajiwa kunyesha ikaleta madhara makubwa iwapo wakazi hawatazingatia tahadhari hiyo na kuyahama maeneo ya mabonde.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Tenga alisema kuwa maafisa wa shirika hilo wametumwa nyanjani kuihamasisha jamii jinsi ya kuepukana na majanga kwani zaidi ya wakazi 3,000 huenda wakaathirika na mvua hiyo iliyotabiriwa kunyesha na idara ya utabiri wa hali ya anga nchini.

“Kama shirika la msalaba mwekundu, kuna mikakati tumeweka japo mvua itatokea kuhakisha kwamba jamii ya Kaunti ya Mombasa haiwezi kupata hatari kama iliyotokea kipindi cha nyuma. Tunakisia watu takribana elfu tatu huenda wakaathirika na mvua hiyo ya El nino lakini tumejiandaa vyema,” alisema Tenga.

Tenga ameyataja maeneo ya Moroto huko Tudor, Kisauni, Likoni, Mishomoroni na sehemu kadhaa za Changamwe kuwa huenda yakaathirika na mvua hiyo na akawataka wakazi kuwa makini zaidi huku akiahidi kushirikiana na serikali ya kaunti kuwasaidia wakazi endapo kutashughudiwa majanga hayo.

“Katika yale maeneo tumeyataja, basi tunatarajia wakazi kuwa na umakini zaidi na kujiepusha na maeneo hayo na pia kuhama maeneo ya juu kwa sababu hatungependa wakazi wasalie katika maeneo ya mabonde na baadaye waathirike na mafuriko,” aliongeza Tenga.

Mvua hiyo ya El nino inatarajiwa kunyesha kwa muda wa kipindi cha miezi mitatu hali ambayo huenda ikasababisha hatari kubwa iwapo wakazi hawatakuwa waangalifu na kujiepusha na mvua hiyo.