Wakazi wa Mtongwe wamelitaka shirika la Feri nchini (KFS) kuwanunulia feri kuwaepusha na masaibu ya kuzunguka hadi Likoni kwa uchukuzi wa feri.
Akiongea siku ya Jumapili katika mtaa wa Mtongwe kwa niaba ya wakazi hao, mwenyekiti wa usalama uhusiano wa wakazi mjini Mtongwe, Suleiman Ramadhan, alidai kuwa wakazi wa eneo hilo wamesahaulika kwa muda mrefu. Alisema wakazi hawa hujihusisha na kazi za vibarua na huwa vigumu kufanikisha mahitaji yao ya nyumbani na inawabidi wengi wao kutembea kwa miguu kutoka eneo hilo la Mtongwe hadi Likoni kila siku kwa kukosa nauli.
Ni umbali wa kilomita 10 kutoka Mtongwe hadi Likoni na wakazi hao wanalalamikia ukosefu wa feri.
Ramadhan aliongeza kuwa serikali ya kitaifa sharti iingilie kati kuleta feri mpya kushughulikia eneo la Mtongwe.
Alihoji kuwa shirika la KFS limewapa mgongo tangu uhuru kwani feri ambazo zimekuwa zikihudumu kwenye kivuko hicho huwa zinahudumu kuwili, kwenye kivuko cha Likoni na kile cha Mtongwe. Wakati mwingine, feri hizo haziji kuwavusha wakazi kunapotokea dharura kwenye kivuko cha Likoni.
Mwenyekiti huyo alishangaa ni vipi shirika hilo la feri linaweza kukosa kununua feri ya watu wa Mtongwe, ilhali shirika hilo hukusanya ada za kuvusha magari na mizigo kila siku kwenye kivuko hicho na kuomba serikali kuukupitia serikali kaunti ya Mombasa kwa ushiriiano na shirika la KFS kufanya hisani na na kuliangazia suala hilo kwa dharura.