Wakazi katika eneo la Keroka wametishia kufanya maandamano ili hatua ya kuweka usalama katika eneo hilo ichukuliwe.
Hii ni baada ya watu watano kuuwawa katika eneo hilo kwa muda wa takribani miezi miwili.
Wakizungumza siku ya Jumatano katika eneo hilo la Keroka, baadhi ya wakazi hao walishtumu maafisa wa polisi kwa kutowajibikia kazi yao na kuimarisha usalama katika mji huo na viunga vyake.
Meroka Ondari ambaye ni mwenyekiti wa wafanyibiashara rejareja katika sehemu hiyo alisema kuwa vijana wasiojulikana wamekuwa wakiwashambulia wakazi wakati wa jioni wanapotoka shughuli zao.
Benson Maina, ambaye ni mfanyibiashara katika eneo hilo, aliwashtumu afisa wa polisi kwa kutojitokeza wakati wanapopiga kamsa wanaposhambuliwa na wahalifu hao ilhali kituo hicho cha polisi hakiko mbali.
"Hatuko hapa kuchinjwa kama kuku ilhali polisi wako hapa karibu. Kama hawatachukua hatua tutaungana tufanye maandamano," alisema Osore Siro, mkazi.
Mmoja wa kikosi cha kuweka usalama katika mji huo Samson Guto aliwataka wakazi wa mji wa Keroka kutotembea pekee yao hasa wakati wa usiku na kuiomba serikali ya kaunti ya Kisii kutatua shida hiyo.
Hata hivyo, OCPD wa kituo cha polisi cha Keroka Fergason Nyongesa aliwatetea maafisa wake huku akisema kuwa wamekuwa wakipiga doria kila siku kwenye mji huo na viunga vyake.
Alisema kuwa mauaji hayo ni miongoni mwa visa vya uhalifu wa kawaida.