Wakimbizi kutoka kaunti ya Kisii huenda wakapata nafuu kwa kulipwa fidia yao ambayo wamekuwa wakipigania tangu baada ya ghasia zilizoikumba nchi ya Kenya mwaka wa 2007/8 baada ya uchaguzi mkuu.
Kulingana na mmoja wa wawakilishi wa wakimbizi hao ambaye amerudi kutoka Nakuru kwenye kikao kilichoandaliwa spesheli kujadili masuala ya fidia, wakimbizi hao watalipwa kufikia mwezi ujao wa Novemba.
Kinara huyo ambaye pia ni katibu wa jumuia ya wakimbizi wote wanaotambuliwa na serikali kuu kutoka kaunti ya Kisii, Alfred Akama alisema kuwa kulingana na masuala ambayo yaliweza kujadiliwa kwenye kikao hicho kilichokamilika siku ya Jumatatu, kuna matumaini kuwa hela zao zitatumwa kwenye akaunti.
Kwenye mahojiano na mshirikishi huyo siku ya Jumatano mjini Kisii, tayari wamewasilisha mapendekezo yao ambayo walikuwa wanalilia na yakakubaliwa, japokuwa yanatarajiwa kupokezwa bunge la seneti ambalo limeweza kujadili awamu ya kwanza ya suala hilo la wakimbizi na baadaye kupewa rais kulikubalia ili walipwe.
Baadhi ya mapendekezo ambayo wakimbizi hao wanataka kuangaziwa, kulingana na wale anaowawakilisha, ni kupata shilingi elfu mia nne ambazo zilikuwa ziwafae kuhamia mahali au kununua ardhi na kuanzisha biashara ili kujiendeleza kiuchumi sawa na wengine kutoka maeneo mengine nchini.
“Upande wetu kama wawakilishi wa wakimbizi na upande uliowakilisha serikali ulishakubaliana, hivyo basi tunangoja usemi wa mwisho kutoka kwa rais wan nchi,” aliongeza Akama.