Share news tips with us here at Hivisasa

Wakimbizi wenye asili ya kisomali wanaodaiwa kutokea katika kambi ya Daadab katika kaunti ya Garissa na kuishi katika eneo la Mji wa Kale mjini Mombasa wanaitaka serikali kuwapa vitambulisho vya kitaifa vya Kenya.

Kulingana na baadhi ya raia hao, wameishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitano na kuahidiwa kupewa vyeti vya kitambulisho vya kitaifa, hatua ambayo bado haijatekelezwa.

Aidha, walisema kwamba wamepitia changamoto nyingi za kuhangaishwa na maafisa wa polisi pamoja na kushukiwa kuwa wafuasi wa wanamgambo wa kundi la kigaidi la Al Shabab, licha ya wao kuwa na stakabadhi muhimu za kuishi humu nchini kisheria.

“Tungependa serikali iingilie kati mambo yetu na itusaidie kupata vitambulisho kwa sababu tuliambiwa tuishi hapa kwa miaka mitano tutapewa vitambulisho kwa sababu polisi wanatuhangaisha sana,” alisema mmoja wa wakimbizi hao siku ya Jumatano mjini Mombasa katika mkutano wa kumasa.

Wakimbizi hao waliitaka serikali kuu kuingilia kati swala lao na kuwasitisha maafisa wa polisi kuwahangisha, pamoja na kuwaitisha pesa, la sivyo watafunguliwa mashtaka mahakamani kwa kuapatikana humu nchini kinyume cha sheria.

“Tunaiomba serikali kuwazuia maafisa wa polisi kukoma kutuhangaisha kila uchao kwa madai ya sisi wakimbizi tuko hapa Mombasa bila stakabadhi halali na vyeti vya kuwa hapa Kenya, tulipewa na tuko navyo, hao polisi ndio hawataki kutuelewa na kutuitisha pesa,” alisema mmoja wa wakimbizi, Fatma Ibrahim.

Wakati huo huo, afisa wa idara inayoshghulikia wakimbizi nchini Fridah Muah amesema kwamba idara hiyo imetangaza kuanzisha zoezi la kuwasajili wakimbizi wanaoingia humu nchini ili kutambua idadi kamili kwani imekuwa vigumu kutambua idadi ya wakimbizi kutoka Somalia wanaoishi katika baadhi ya miji nchini ikiwepo mji wa Mombasa.