Baada ya subira ya mda mrefu, huenda sasa wakimbizi wa baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007/8 kutoka kaunti ya Kisii wakapata suluhu la kudumu kuhusiana na malalamiko ya fidia ambayo wamekuwa wakipigania kortini.
Katika kesi hiyo ambayo ilisikilizwa siku ya Jumatatu katika mahakama kuu ya Kisii mbele ya hakimu mkuu Crispine Nagila, wakimbizi hao zaidi ya 100 waliombwa na mahakama kuwasilisha malalamishi yao ndani ya siku saba, huku mashauri mkuu wa masuala ya kisheria wa serikali akipewa jumla ya siku saba kutoa tetesi zake ndipo uamuzi ufanywe.
Wakimbizi hao walipewa jumla ya siku 30, ambapo korti itaangazia mawasilisho yao na yale ya upande wa serikali, ndipo hakimu huyo atatoa uamuzi kuhusiana na maafikiano ya pande mbili husika.
Akiongea siku ya Jumatatu baada ya kusikilizwa kesi hiyo kwa niaba ya wakimbizi hao, msemaji wao Nemuel Momanyi alitoa matumaini yake kuwa watafidiwa kama wengine walivyolipwa na kujiendeleza maishani.
Aliongeza kusema kuwa wanaamini korti itazingatia kilio chao na kufanya uamuzi unaowafaa, ambapo aliwaomba viongozi kutoka Kisii kuwaunga mkono ili nao wajiendeleze kama wengine ambao waliathirika mwaka 2007.
Ikumbukwe kwamba kesi hiyo imekuwa ikishughulikiwa kwa miaka saba sasa na bado lawama zimekuwa kwa baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitumia masaibu ya wakimbikizi hao kujifaidi.