Share news tips with us here at Hivisasa

Zaidi ya wakimbizi wa ndai kwa ndani 60 walioathirika kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008 ambao wangali katika kambi ya Kamwingi-Yamumbi mjini Eldoret wameelezea hofu ya kutokea maafa katika kambi yao wakati wa mvua ya El Nino.

Wakimbizi hao walisema mvua hiyo ambayo inatarajiwa nchini wakati wowote itasababisha maafa makuu katika kambi hiyo kutokana na ubovu wa mahema na mazingira duni ambamo wanaishi.

Wakimbizi hao walitaka serikali kuwafidia na kuwaondoa katika kambi hiyo kabla ya athari za El Nino kuanza kushuhudiwa kote nchini.

Mwenyekiti wa kambi hiyo Bi Ruth Nduta alisema kambi hiyo inatishiwa na mkurupuko wa maradhi na kusombwa na mafuriko.

Akizungumza na wanahabari kambini humo siku ya Alhamisi, Bi Nduta alisema mahema yao yamejengwa katika ardhi ya Chemichemi ambayo walipewa na msamaria mwema hivyo basi kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mafuriko.

Bi Nduta aliitaka serikali kuwanusuru kwa kuwapa makao mbadala kabla ya mvua husika kuanza kunyesha.

Msamaria mwema ambaye aliwapa wakimbizi hao mahala pa kujenga mahema yao baada ya kutolewa katika iliokuwa kambi kuu ya Yamumbi, Askofu Peter Ndung’u wa Living Water Church of Christ ameunga mkono kilio chao.

“Hofu yangu sio wakati watakaolipwa, lakini serikali inapaswa iangalie maafa ambayo yanaweza yakutapata kutokana na hali ya wakimbzi hawa wa ndani kwa ndani,” alisema Ndung’u.