Share news tips with us here at Hivisasa

Wafugaji wametakiwa kuchukua jukumu la kuangalia afya ya mifugo wao kwa kuwatibu angalau mara moja kwa kila wiki.

Kwenye mahojiano na mkurugenzi mkuu wa Idara ya Matibabu ya Wanyama katika kaunti ya Kisii siku ya Alhamisi, Moenda Omwoyo, alisema kuwa wakulima wengi kwenye kaunti hiyo wameasi na kukomesha utaratibu wa kuwatibu wanyama wao.

Aliwasihi wakulima kuanza kuungana kwa makundi na kununua dawa kwa jumla ili kutibu mifugo wao badala ya kusema hawana pesa.

Omwoyo alisema kuwa wafugaji sharti watoke enzi za kulishwa kila kitu na serikali huku akisema kuwa lazima wakulima wajiunge katika vikundi kama vya watu kumi ili kufanya mchango na kununua dawa za kunyunyuzia wanyama wao.

“Wadudu kama kupe ni hatari sana hasa wakikosa kumwagiwa dawa. Wadudu hao humfanya mnyama kama ng’ombe kupunguza kiwango cha maziwa na hata husababisha ng’ombe kufa wakiwa wengi kwenye mwili wake,” alisema Omwoyo.

Aidha, aliwataka wafugaji wawe wakihudhuria hafla mbali mbali ambazo huandaliwa kila mwezi kwa mafunzo ya wafugaji.

Aliwataka wakulima wamakinikie kazi yao ndio uchumi wa kila mkazi wa Kaunti ya Kisii uimarike ikizingatiwa kuwa kazi za ofisi ni finyu kupatikana.