Wakulima katika eneo la Seme, Kaunti ya Kisumu wametakiwa kulima mchanganyiko wa vyakula vya kiasili na kuzalisha mazao ya nafaka kwa wingi ili kudhibiti makali ya njaa.
Mwenyekiti wa bodi inayosimamia kilimo katika Wadi ya Seme Mashariki, Andrew Aroko amewahimiza wakulima wa eneo hilo kuzingatia sana kilimo cha vyakula kama vile mihogo, viazi vitamu, mtama na wimbi vilivyo asili ya vyakula katika kanda ya Nyanza.
''Watu wetu wameacha kulima vyakula vya kienyeji ambavyo vinaweza kudhibiti makali ya njaa, na hivyo basi tunahimiza kila mmoja katika eneo hili kujaribu kurejelea kilimo cha vyakula vya kiasili,'' alisema mwenyekiti huyo kwenye kikao maalumu na wakulima mnamo siku ya Jumamosi.
Aroko alidokeza kuwa chakula hicho kikizalishwa kwa wingi basi eneo hilo litashuhudia maendeleo makubwa, akisema kuwa mbali na kudhibiti makali ya njaa, wakulima watatengeneza donge nono la pesa, ikizingatiwa kuwa vyakula asili vinatatikana sana nchini.
Aidha, Aroko alisema kuwa vyakula vya kiasili huchangia madini muhimu kwenye mwili, ikilinganishwa na vyakula vya kigeni.
Aliongezea kwamba vyakula hivyo vina manufaa mengi mwilini, ikiwemo kukinga magonjwa na kuongeza damu.