Chama cha wakulima wa majani chai cha 'Gucha Alliance', kinachotetea haki na uwazi wa wakulima wa mmea huo katika kaunti ya Kisii kimelalamikia pesa wanazolipwa kwa kila kilo la zao lao.
Kulingana na chama hicho, kuna ufisadi hufanywa na wakurugenzi wa viwanda mbalimbali vya kusiaga majani chai yao na kuuza zao lao kwa pesa nyingi huku wakiendelea kuwanyanyasa wakulima kwa kuwalipa pesa kwa kiasi kidogo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika eneo la Eberege, mwenyekiti wa chama hicho Jimmy Momanyi alisema uchunguzi ambao umefanywa unaonyesha kuwa majani chai yao huuzwa kwa pesa nyingi ikilinganishwa na zile wanalipwa hapa Kenya baada ya majani chai yao kuuza kwa nchi za ng’ambo kwa bei ya juu.
Kulingana nao, wakurugenzi wa viwanda vya majani chai katika eneo la Gusii hutajirika pindi wanapoingia uongozini, jambo ambalo wamesema ni kunyanyaswa kwa wakulima na kuwalipa pesa zao za majani chai hayo.
“Bei ya majani chai yetu ambayo inauzwa kule ng’ambo ni tofauti na bei ile tunaletewa hapa Kenya ya shillingi nane hadi 15 ni tofauti, inamaanisha wengi wamejitajirisha kupitia jasho la wakulima na hilo hatutaliruhusu kuendelea kamwe,” alisema Momanyi.
Aidha, wakulima hao wamekosoa chama cha KTDA kwa kumiliki wakurugenzi ambao ni wafisadi, na ambao hawajali maslahi ya wakulima kwa kuendea 'kuwaibia'.
Kwa upande wake, naibu mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni wakili Nyamwango Oigara aliikosoa KTDA kwa kutochukua majani chai kutoka kwa vituo vya kupima, na kusababishia wakulima hasara kubwa kwa kupoteza wakati wao kusubiri kupima majani chai.
“Wakulima huendelea kunyanyaswa na kusalia katika hali ya umaskini hilo hatutaki kamwe wakati wengine wanapoendelea kujitajirika kwa jasho letu,” alisema Oigara.