Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mshauri wa masuala yakifedha wa benki ya dunia tawi la Kenya, Bw Charles Mochama amewaomba wakulima wa majani chai katika Kaunti ya Nyamira kuomba mikopo kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika ili kujiendeleza kimaisha.

Akizungumza kwenye kiwanda cha usagaji chai cha Nyankoba siku ya Jumanne, katika mkutano wa washikadau, mshauri huyo aliwaomba wakulima kuchukua mikopo kutoka kwenye benki za kibiashara za Family Bank na ile ya Equity mahala ambapo alisema kuwa benki ya dunia imeekeza pakubwa ili kuwawezesha wakulima kupokea mikopo ya faida ya asilimia nane pekee.

"Nawaomba wakulima wote wa majani chai kwenye Kaunti ya Nyamira kuchukua mikopo kutoka kwenye benki za Family na Equity watakazolipa kwa faida ndogo ili waweze kujiimarisha kimaisha,” alisema Mochama.

Mochama aidha aliwaomba wakulima kutotegemea kilimo cha chai pekee huku akiwasihi kujaribu kilimo cha nyanya na vitunguu ili kuongeza mapato yao.

"Ningependa kuwasihi wakulima kutotegemea tu kilimo cha chai na wajaribu kuanzisha kilimo cha mimea mingine kama vile nyanya na vitunguu ili kuimarisha mapato yao ya kila siku,” alisema Mochama.