Wakulima wa mboga na matunda katika Kaunti Ndogo ya Muhoroni wametakiwa kuzingatia mawaidha ya wataalamu wa kilimo ili kuongeza mazao yao.
Bi Rachel Omolo ambaye ni Mtaalamu wa kilimo hicho kutoka Wizara ya kilimo kaunti hiyo ndogo, aliwaambia wakulima katika eneo hilo kubadilisha kutoka mfumo wa zamani na kuegemea kilimo cha kisasa ili kufurahia mazao mazuri.
Akizungumza kwenye kikao cha kuhamasisha wakulima kilichoandaliwa katika Kata Ndogo ya Tamu siku ya Alhamisi, Omolo aliwaelezea wakulima hao kuwa kuna haja ya kuhamia kwenye mfumo mpya wa kilimo ili kupata mazao mengi.
"Siku hizi kila kitu kimebadilika, iwe ni biashara au kilimo kama kazi ile nyingine tunastahili kutumia mbinu mpya na za kisasa ili tuweze kupata faida," alisema Omolo.
Aidha, mtaalamu huyo aliwataka wakulima hao kutia bidii katika kuhudhuria vikao vya kutoa alimu ya bure kwa wakulima kinachoandaliwa na serikali ya Kaunti ya Kisumu kila baada ya miezi mitatu na pia kuwapokea wataalamu wanaozuru wadi za eneo hilo kila mwezi.
Wakulima hao walielezea hasara wanazopata kila msimu kutokana na kuharibika kwa mimea yao kwenye mashamba. Walidokeza kuwa mbali na kupata mazao duni kwenye kilimo hicho, mboga na matunda huoza kwa wingi vikiwa vingali katika mashamba. Aidha waliomba serikali ya Kaunti ya Kisumu kuwasambazia dawa za msaada ili kunyizia mimea yao inayooza kwa kushambuliwa na wadudu haribifu.