Katika hatua mojawapo ya kuwapa nguvu wakulima wa miwa katika eneo bunge la Mogirango Kusini, wizara ya kilimo imeanza uhamasisho miongoni mwa wakulima kutoka eneo hilo kujiandikisha kwenye makundi ya jumuia.
Hatua hiyo itafanya iwe rahisi kwao kuweka mwafaka kati yao na kampuni za kusaga miwa.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika afisi yake, waziri wa Kilimo Bwana Vincent Sagwe, alisema kuwa wakulima wakiwa katika vyama itakua rahisi kupata mikopo.
Aliwataka wakulima kupanda miwa kwa wingi ili ziwafae kimapato na kuendeleza uchumi wa eneo hilo ambalo limesahaulika kwa muda mrefu.
Sagwe alisema hii ni nafasi yao ya pekee ya kupata kazi katika viwanda kama hivyo.
Dhamira hii inalenga zaidi kiwanda cha miwa ambacho kitajenywa katika eneo bunge hilo sehemu ya msitu wa Nyangweta hivi karibuni.
Waziri huyo alisema kuwa wakaazi wa eneo hilo watafaidi mno wakiwa na chama kimoja cha kuwasilisha miwa kwenye kiwanda hicho.
"Tumewaambia wakulima wa miwa kuunda makundi ili wawe na maandalizi thabiti kabla ya kiwanda kuanza kazi rasmi. Itakuwa rahisi kujadili bei ya miwa yao wakiwa jumuia," alisema waziri huyo.
Kiwanda hicho cha sukari tayari kimewekewa msingi na huenda ujenzi wake utaanza kabla ya mwisho wa mwaka.
Serikali ya kaunti ya Kisii ilikwishalaza roho za baadhi ya waasi miongoni mwa wakaazi ambao walikuwa wakipinga uwepo na ustawishaji wa kiwanda hicho huku wakidai kuwa kitawadhuru kiafya.