Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima kutoka eneo la North-Rift wameelezea hofu ya mashirika ya umma ya wakulima kuendelea kubinafsishwa.

 

Wakulima hao wamesema licha yao kupinga kubinafsishwa kwa kiwanda cha maziwa cha KCC mjini Eldoret, hakuna hatua yeyote ambayo imechukuliwa ili kushughulikia kilio chao.

 

Wakihutubu katika maadhimisho ya siku ya Mashujaa mjini Eldoret, viongozi wa wakulima hao walisema kuna njama ya kubinafsisha mashirika yote ya wakulima.

 

Mwenyekiti wa chama cha wakuzaji nafaka nchini mzee Musa Barno alisema ni kinaya kuona kwamba wakulima hawatambuliwi nchini kama mashujaa.

 

Barno alisema miongoni mwa njia za kutambua wakulima kama mashujaa ni kurejesha kampuni ya KCC mikononi mwa wakulima.

 

Mbali na kulilia KCC, Barno alitaka serikali kutoa usimamizi wa bodi ya nafaka na mazao nchini NCPB kwa wakulima, huku akisema iwapo wakulima watapewa usimamizi wa NCPB, watatunza bodi hiyo kwa njia nzuri ikizingatiwa kuwa wanafahamu umuhimu wake.

 

“Sisi kama wakulima tunataka mchakato wa kurudisha usimamizi wa KCC mikononi mwa wakulima kuendelea kwa lengo la kutaka wakulima kutwikwa majukumu ya kusimamia kiwanda hicho,” alisema Barno.

 

Naye mkurugenzi wa shirikisho la wakulima, KFA, Kipkorir Menjo alitaka serikali kutumia sehemu kubwa ya fedha za kukabiliana na athari za mvua ya El Nino kutengewa wakulima kwa ununuzi wa mahindi.

 

Menjo alisema shilingi 2.7 bilioni ambazo zimetengewa NCPB kununua mahindi kutoka kwa wakulima ni kidogo mno, ikilinganishwa na mavuno ambayo wakulima wanatarajia kupata mwaka huu.

 

“Shilingi 2.7 bilioni ambazo zimetengewa NCPB kununua mahindi ni kidogo sana ikilingansihwa na takribani magunia milioni 10 ya mahindi ambayo wakulima wanatarajia kuvuna,” alisema Menjo.

 

Menjo alipendekeza kuwa fedha ambazo serikali imetenga kukabiliana na athari za mvua ya El Nino zitolewe kwa NCPB kununua mahindi kutoka kwa wakulima.