Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikiali imeombwa kusambaza mbolea kwa wakulima kabla ya muda wa upanzi kuyoyoma ili mazao ya wakulima yawe mema.

Hii ni baada ya wakulima wengi katika eneo la Gusii kuendelea kutayarisha mashamba yao wakiwa na nia ya kupanda mapema ili kukabiliana na janga la njaa.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumapili wilayani Marani kaunti ya Kisii, wakulima hao wakiongozwa na peter Monari waliomba wizara ya Kilimo katika eneo hilo kufanya mipango na harakati za mapema ili kuwakabidhi mbolea na mbegu.

Haya yanajiri baada ya idadi kubwa ya wakulima katika eneo hilo kupata mavuno duni ikilinganishwa na mavuno ya msimu uliopita.

Wakulima hao walisema kuwa mavuno hayo yalikuwa duni kutokana mvua nyingi iliyosababisha mashamba yao kujaa maji na kusomba mimea.

“Tumejitayarisha kikamilifu msimu huu maana wengi wetu tunaendelea na matayarisho ya upanzi ili tujiepushe na uharibifu wa mimea yetu,” alisema Joshua Osao mkulima wa mahindi Kisii.

Aliongeza: “Tunaomba serikali iharakishe kutupatia mbolea na mbegu ili tuweze kupanda mimea yetu mapema.”