Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima kutoka Kaunti ya Kisii wameshauriwa kufanya kilimo kama taaluma na kupanda mseto wa mimia inayokuwa kwa haraka.

Hatua hiyo inalenga kupunguza njaa na kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo ili kuwa na chakula cha kutosha kwa wakazi pamoja na nchi kwa jumla.

Hii ni baada ya kubainika kuwa wengi wa wakazi kutoka eneo zima la Gusii wamekuwa wakifanya ukulima kama chaguo la pili na kwa hiari ya kulisha jamii na familia, bila kuzingatia umuhimu wa kufanya biashara kilimo ili chakula cha ziada kutumiwa kama kitega uchumi kwenye maboma ambayo yana utegemezi mkubwa kwenye ukulima.

Akizungumza siku ya Jumatano, mwenyekiti wa shirikisho moja la wakulima ambalo hujihusisha na ukuzaji na uuzaji wa mazao ya asilia na yale ya kisayansi kutoka maeneo ya Gusii, Bwana Nyachae Abuya, alisema kuwa wengi wa wakulima kutoka kaunti za Kisii na Nyamira wamekuwa na mazoea ya kupanda aina moja au mbili za mimea, hali ambayo imesababisha eneo zima la Gusii kukumbwa na baa la njaa na ukosefu mkubwa wa vyakula.

Alisihi wakulima kuanza kupanda mimea ambayo hustahimili hali mbaya ya misimu kama ile ya kiangazi na ile ya kukua kwa muda mfupi.

“Upungufu huo umekuwa chanzo kikuu cha kupandishwa bei ya kununua vyakula kama vile mahindi ambayo kwa muda mrefu yalikuwa yanazalishwa kwa wingi katika eneo la Gusii,” alisema Abuya.

Alishauri wakulima kuhudhuria vikao vinavyoandaliwa na makundi mbali mbali ya wakulima kwa ushrikiano na wizara za kilimo za serikali kuu za ile ya kaunti kupitia idara husika za kilimo ili kujipatia maarifa na ujuzi jinsi ya kufanya ukulima wa kisasa na kupanua hali ya kupata mapato kupitia kilimo.