Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Idadi kubwa ya watu wanaoishi na ulemavu wanaojikimu kwa kuombaomba jijini Mombasa wanahofia kuathirika na njaa msimu huu wa El Nino.

Walisema kuwa huenda wakakosa chakula ikizingatiwa kuwa maeneo wanayoendeleza harakati zao hufurika wakati wa mvua.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Karisa Babu, mzee wa miaka 70 ambaye anaishi na ulemavu alisema kuwa mvua ya El Nino itawaathiri pakubwa ikizingatiwa wanaishi kwa kuomba wapita njia ambao watapungua msimu huu wa mvua.

Karisa aliitaka serikali kushughulikia pakubwa maswala ya watu wanaoishi na ulemavu hasa msimu huu wa mvua ili waweze kupata riziki.

“Hali yetu ya maisha itakuwa ngumu msimu huu wa El Nino. Sijui nitapata wapi riziki ikizingatiwa hapa nilipokaa hufurika wakati wa mvua,” alisema Karisa.

Aidha, aliongeza kuwa itakuwa vyema iwapo wanaoishi na ulemavu watafunguliwa biashara ili waacha mtindo huo wa kuomba jijini.