Tume ya kuajiri walimu nchini TSC imelaumiwa kwa kuwapa uhamisho baadhi ya walimu kutoka eneo la Masaba kwa kuwaonea walimu hao kinyume na sheria.
Akiongea kwenye shule ya upili ya mseto ya Don Bosco Nyabiosi siku ya Jumatatu, katibu mkuu wa chama cha kutetea maslahi ya walimu Knut tawi la Masaba Meshack Ombong'i alisema kuwa baadhi ya walimu tayari wamewasilisha lalama zao kwenye afisi yake, huku akiongezea kusema kuwa uhamisho wa walimu haufai kutekelezwa kwa kuwabagua walimu wengine na hata pia kutopeanwa sababu mwafaka za uhamisho wa aina hiyo.
"Afisi yangu tayari imepokea lalama nyingi za uhamisho wa ubaguzi na tayari tumeanzisha uchunguzi wa kesi 15 za uhamisho wa walimu zilizoripotiwa mwezi oktoba mwaka huu, na iwapo tume ya TSC inafanya hivyo bila ya sababu mwafaka, lazima isitishe hilo kwa haraka," alisema Ombong'i.
Ombong'i aliongeza kusema kuwa uhamisho huo wa lazima huathiri utendakazi mzuri wa walimu, hali inayosababisha hata wanafunzi wa shule wanakohamishiwa kutofanya vizuri kwenye mitihani.
"Hali hiyo ya kuwahamisha walimu kwa lazima huathiri sana utendakazi wa walimu hali inayosababisha wanafunzi wa shule wanakohamishiwa walimu hao kutofanya vizuri kwenye mitihani yao na kwa sababu hiyo, tume ya TSC yafaa kuwapa walimu uhamisho kwa uwazi na haki," aliongezea Ombong'i.
Afisa huyo wa Knut aidha alisema kuwa lalama nyingi za walimu waliohamishwa zinatoka na tofauti za kibinafsi baina yao na walimu wakuu wa shule, swala ambalo chama hicho kinalipinga vikali.
"Uhamisho wa walimu wengi husababishwa na tofauti ndogo ndogo baina ya walimu na walimu wakuu wa shule, swala ambalo tunalipinga vikali na tayari tushaiandikia barua tume ya uajiri wa walimu TSC kuhusiana na swala hilo," alisema Ombong'i.