Walimu wa shule za binafsi katika wilaya ya Kisii Kusini, kaunti ya Kisii wamepewa siku moja kufunga shule na kujiunga na mgomo unaoendelea wa walimu wa shule za umma au kama sivyo wawe tayari kukabiliana na walimu wanaogoma.
Onyo hilo limetolewa na zaidi ya walimu elfu moja ambao walikuwa wakishiriki mgomo katika mji wa Suneka na vyunga vyake siku ya Jumatatu, baada ya serikali kudinda kuwalipa nyongeza ya kati ya asili mia 50-60 ilivyoagizwa na mahakama.
Akiongea kwa niaba ya walimu wakati wa maandamano hayo, katibu mkuu wa chama cha kuwatetea walimu cha Knut katika tawi la Kisii Kusini Charles Mokua alisema kuwa si haki wanafunzi wa shule za binafsi kuendelea kufunzwa huku wenzao wa shule za umma wakiendelea kuwa nje, na kuwataka walimu wa shule hizo kuwa tayari na kushikana mikono na kuanza kuandamana na wao ili haki ipatikane kwa walimu.
Alisema kuwa walimu wa shule za binafsi watakuja kuajiriwa na serikali, na ndio sababu wanapigania haki ya walimu wote bila kubagua.
“Walimu wa shule za binafsi na wenye shule hizo sharti wajiunge na sisi katika hizi harakati za kupigania haki za walimu wetu, sababu hata walimu wa shule hizo walisomea ualimu na wakiwahi kuajiriwa na serikali, tunataka wapate mshahara wa kukimu mahitaji,” alisema katibu huyo.
Matamshi yake yaliungwa mkono kwa sauti moja na walimu hao ambao walizunguka takribani kila shule ya umma na zile za binafsi ili kuwapa ujumbe wa kushiriki mgomo huo.