Huku mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne na darasa la nane kote nchini ikitarajiwa kuanza mwezi huu, wanafunzi na walimu wahimizwa kuondoa hofu ya ukosefu wa usalama.
Kulingana na Mkurungenzi mkuu wa Tume ya Kuajiri Walimu nchini TSC tawi la Mombasa Ibrahim Rugut, maafisa wa usalama wametumwa katika kila shule katika kaunti hiyo kushika doria saa 24 ili kuona kwamba usalama wa wanafunzi unaangaziwa kikamilifu.
Akiongea na wanahabari katika afisi za tume hiyo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Rugut alisema kwamba wamechukua hatua hiyo kutokana na hofu miongoni mwa wanafunzi kwamba huenda baadhi ya shule zikashuhudia usumbufu wakati wa mitihani hiyo.
“Kama tume ya kuajiri walimu tukishirikiana kwa karibu mno na Wizara ya Elimu nchini, hasa katika kaunti ya Mombasa, tunawahakikishia wanafunzi usalama dhabiti na mitihani itafanyika bila pingamizi zozote,” alisema Rugut.
Aidha, aliwahimiza wakazi, walimu pamoja na wanafunzi kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu ama watu wanaopanga njama za kutatiza shughuli za masomo pamoja na mitihani hiyo ya kitaifa ili wakabiliwe na maafisa wa polisi.
“Tunawaomba wazazi, walimu na wanafunzi kujitokeza waziwazi na kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu wanaopanga njama ya kuvuruga mitihani hiyo pamoja na kusambaratisha shughuli za masomo ili wakabiliwe na maafisa wa usalama,” alisema Rugut.
Haya yanajiri baada ya tetesi kuwa kuna baadhi ya watu fulani wanapanga njama ya kuvuruga mitihani hiyo ya kitaifa katika kaunti hiyo kwa madai kuwa tume hiyo imekosa kuwalipa walimu nyongeza yao ya asilimia 50 hadi 60 pamoja na mishahara yao ya mwezi Septemba.