Mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti ya Kisii Richard Chepkawai, amewaonya walimu dhidi ya kushiriki masomo ya likizo.
Chepkawai alisema kuwa walimu watakaopatikana wakiwaruhusu watoto kuenda na kushiriki masomo ya shule wakati huu wa likizo watachukuliwa hatua kali na serikali.
Akizungumza ofisini mwake siku ya Jumanne, Chepkawai alisema kuwa ni kinyume na sheria ya wizara ya elimu kuwakubalia wanafunzi kuenda shuleni kusoma ilhali ni wakati wa wanafunzi hao kupata muda wa kupumzika na kurejelea masomo yao baada ya likizo.
Mkurugenzi huyo aliwataka wazazi pamoja na umma kutoa ripoti iwapo kutakuwa na shule yoyote ambayo itakuwa inaenda kinyume cha sheria kwa kuwatoza ada za kushiriki masomo ya ziada yaliyoharamishwa
“Ningependa kila mwanafunzi apewe muda wa kutosha ili apumzishe akili. Huu si muda wa kusoma. Sharti wazazi na walimu wazingatie msimamo na sheria ya wizara ya elimu kuwa wanafunzi wasipatikane wakienda shuleni nyakati za likizo,” alisema Chepkawai.
Alisema kuwa masomo hayo ya likizo yamekuwa kisingizio kwa wengi wa walimu ambao wamekosa kuwajibikia kazi ya kufundisha na kungojea hadi likizo na kuanza kuwatoza pesa wanafunzi pesa ndio wawafundishe.
Chepkawai alisema kuwa mtindo huo umekita mizizi nchini na kuwa ni hatari kwa jamii kwani baadhi ya walimu wanatumia likizo kama biashara kwa kutoza hela nyingi ilhali wengine ni waajiriwa wa tume ya kuwaajiri walimu TSC.