Mwenyekiti wa kitaifa wa Nyumba Kumi nchini Joseph Kaguthi amesema kwamba ili usalama kuimarishwa na kusitishwa kwa visa vya kigaidi nchini, serikali inafaa kuwapa bunduki walinzi wa kibinafsi.
Kulingana na Kaguthi, iwapo serikali italipuuza swala hilo, basi taifa hili litazidi kukumbwa na changamoto za kiusalama kwani walinzi hao hutoa ulinzi kwa wananchi wengi, na ni kujumu la serikali kupitia kwa wizara ya usalama wa ndani nchini kuandaa mpango huo.
Akizungumza na wanahabari baada ya kuhudhuria kongamno la kiusalama katika ukumbi wa taasisi ya mafunzo ya kiserikali mjini Mombasa siku ya Jumanne, Kaguthu alisema kwamba iwapo wizara hiyo ya usalama itashirikiana vyema na waajiri wa walinzi hao na kuzindua mapango wa mafunzo ya kutumia bunduki, basi wakenya wataisha bila hofu.
“Serikali inafaa kuliangazia vyema swala la usalama nchini na kuandaa mpango wa kuwapa mafunzo walinzi wa kibinafsi kote nchini ili wapewe bunduki na kuimarisha usalama kikamilifu, kwani hatua hiyo naona itasaidia pakubwa kudhibiti visa vya kigaidi na uhalifu nchini,” alisema Kaguthi.
Aidha, amewashinikiza wakazi kushirikiana vyema na maafisa wa usalama katika kutoa habari kuhusu washukiwa wa uhalifu na magaidi ili kutiwa nguvuni.
Wakati huo huo, afisa huyo alipendekeza kuimarisha kwa mpango wa Nyumba Kumi mashinani ili kuona kwamba wananchi wanawatambua vyema wageni wanaoingia katika makazi yao sambamba na wale wahalifu na kuwaripoti kwa maafisa wa usalama na kutiwa nguvuni.